Wednesday, February 8, 2017

Askofu mstaafu wa kanisa la Pentekoste
(FPCT) Singida mjini Dk. Paul Samweli,
amesema suala la serikali ya Dk. John
Magufuli kusisitiza ulipaji wa kodi na
ushuru ni utekelezaji wa maagizo ya
Yesu Kristo, hivyo waumini na
Watanzania kwa ujumla, wanatakiwa kutii
na kuzingatia wajibu wao huo.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo,
amesema kwa mujibu wa kitabu
kitakatifu cha Mungu cha biblia Warumi
13 (msitari 1-14), inaonesha wazi Yesu
kristo alipigia debe Mamlaka ya mapato
Tanzania (TRA).
Askofu Paul alisema katika Warumi 13
kimeainisha kuwa watoza kodi na
ushuru, ni wahudumu wa Mungu kuwa
wapeni haki zao, mtu wa kodi, kodi, mtu
wa ushuru, ushuru.
Dk. Paul amesema hayo juzi wakati
akihubiri kwenye ibada ya kawaida
ambayo pia ilihudhuriwa na kamanda wa
jeshi la polisi mkoa mkoani hapa ACP
Debora Daudi Magiligimba.
Akisisitiza, alisema kwa vile ulipaji kodi
umepewa baraka zote na Mwenyezi
Mungu, waumini wa madhehebu
mbalimbali ya dini, wanapaswa kuwa
mstari wa mbele katika kutii agizo la
Mungu la kulipa kodi uliowekwa kisheria
bila shurti.
“Serikali ya Rais Magufuli katika hili la
uhimizaji wa ulipaji kodi na ushuru,
inafanya vizuri kazi iliyopo mbele yetu
waumini wa dini na Watanzania kwa
ujumla, ni kulipa kodi na ushuru kwa
wakati, ili nchi yetu iweze kusonga mbele
kimaendeleo. Haya mambo ya kukwepa
kulipa kodi au ushuru, yakomeshwe,”
alisema.
Kuhusu watoza kodi na ushuru Dk.Paul,
alisema kuwa katika Biblia (Luka
Mtakatifu 3 -12-17) inasema watoza
kodi/ushuru waliagizwa wasitoze kubwa
ambayo itakuwa kinyume na sheria
inavyoagiza.
Akifafanua, alisema wafanyakazi wa TRA,
katika utekelezaji wa majukumu yao,
wanatakiwa kutoza kodi na ushuru kwa
mujibu na sheria, kanuni na taratibu
zilizowekwa na si vinginevyo.
“Wakitoza kodi au ushuru mkubwa ambao
upo kinyume na sheria, watakuwa
wanamudhulumu mlipaji, kitendo hicho
sio tu binadamu mwenye maadili mema
hakipendi, lakini pia, nacho
hakitampendeza Mwenyezi Mungu,”
alisema.
Kwaupande wa jeshi la polisi, Dk. Paul
amesema kwamba katika kitabu cha
Warumi 3 mstari wa 14, kimewataka
askari polisi katika kutekeleza majukumu
yao, wasidhulumu mtu wala
wasiwababikizie watu kesi za uongo. Pia
watosheke na mshahara wanaolipwa.
“Kamanda maneno yaliyotamkwa na
mtumishi wa Mungu Yohana, yanamtaka
kila askari polisi, aridhike na mshahara
wake. Ina maana asiwe na tamaa ya
kuomba rushwa na vile vile asibabikie
mwananchi kesi, bali atatekeleza wajibu
wake kwa mujibu wa mkataba wake wa
kazi,” alisema.
Dk. Paul alitumia fursa hiyo kulipongeza
jeshi la polisi mkoa wa Singida kwa
juhudi zake za kudhibiti vitendo vya
kihalifu ambavyo vinaweza kuhatalisha
amani na utulivu ulipo.
“Nikupongeze kipekee kamanda
Magiligimba kwa kuazisha utamaduni
mpya wa kuongea na waumini wa
madhehebu ya dini kwenye nyumba zao
ibada. Pia kwa uamuzi wako wa kudhibiti
uhalifu kabla haujatokea. Kwa kifupi
unataka dalili za kutokea uhalifu,
zishughulikiwe mapema kabla hazijaleta
madhara. Sisi kanisa tunakuunga mkono
katika hili. Mungu akutangulie,” alisema
Dk.Paul.

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.

Popular Posts

Our Facebook Page

Video